Sura ya 88 kati ya 114 · Makkiya

Sura Al-Ghashiya (Tukio Lifunikalo)

سُورَةُ الغَاشِيَةِ
Aya 26

Tafsiri ya maana: Ali Mohsin Al-Barwani, QuranEnc.com, toleo 1.0.1. Tafsiri huwasilisha maana za Qur'ani. Qur'ani yenyewe ni maandishi ya Kiarabu.

بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1
هَلْ أَتَىٰكَ حَدِيثُ ٱلْغَـٰشِيَةِ
Je! Imekufikia khabari ya msiba wa kufudikiza? [1]
Maelezo ya chini[1] Je! Ewe Muhammad! Imepata kukujia hadithi ya Kiyama ambacho kwa vitisho vyake kitawafanya watu wazimie?
Kiungo 88:1
2
وُجُوهٌۭ يَوْمَئِذٍ خَـٰشِعَةٌ
Siku hiyo nyuso zitainama! [2]
Maelezo ya chini[2] Siku hiyo ya Kiyama zitakuwepo nyuso zimedhalilika,
Kiungo 88:2
3
عَامِلَةٌۭ نَّاصِبَةٌۭ
Zikifanya kazi, nazo taabani. [3]
Maelezo ya chini[3] Zimechoka, taabani kwa shughuli na mashaka ya Motoni,
Kiungo 88:3
4
تَصْلَىٰ نَارًا حَامِيَةًۭ
Ziingie katika Moto unao waka . [4]
Maelezo ya chini[4] Zinaingia kwenye Moto unao waka kwa nguvu!
Kiungo 88:4
5
تُسْقَىٰ مِنْ عَيْنٍ ءَانِيَةٍۢ
Zikinyweshwa kutoka chemchem inayo chemka. [5]
Maelezo ya chini[5] Wananywesha maji yanayo toka kwenye chemchem inayo tokota.
Kiungo 88:5
6
لَّيْسَ لَهُمْ طَعَامٌ إِلَّا مِن ضَرِيعٍۢ
Hawatakuwa na chakula isipo kuwa kichungu chenye miba. [6]
Maelezo ya chini[6] Hawana chakula ila chakula kiovu kabisa, anaadhibika mwenye kukila.
Kiungo 88:6
7
لَّا يُسْمِنُ وَلَا يُغْنِى مِن جُوعٍۢ
Hakinenepeshi wala hakiondoi njaa. [7]
Maelezo ya chini[7] Hakileti nafuu yoyote katika mwili, wala hakiondoi njaa.
Kiungo 88:7
8
وُجُوهٌۭ يَوْمَئِذٍۢ نَّاعِمَةٌۭ
Siku hiyo nyuso nyengine zitakuwa kunjufu. [8]
Maelezo ya chini[8] Na pia zitakuwapo nyuso zenye kutoa nuru Siku ya Kiyama, kwa malipo ya vitendo vyao walivyo fanya duniani.
Kiungo 88:8
9
لِّسَعْيِهَا رَاضِيَةٌۭ
Zitakuwa radhi kwa juhudi yao! [9]
Maelezo ya chini[9] Hao watakuwa wameridhia kwa watayo yapata katika Pepo iliyo juu kwa pahala na cheo.
Kiungo 88:9
10
فِى جَنَّةٍ عَالِيَةٍۢ
Katika Bustani ya juu. [10]
Maelezo ya chini[10] Katika Pepo iliyo juu kwa pahala na cheo.
Kiungo 88:10
11
لَّا تَسْمَعُ فِيهَا لَـٰغِيَةًۭ
Hawatasikia humo upuuzi.Humo imo chemchem inayo miminika. [11]
Maelezo ya chini[11] Humo halisikilizani neno la upuuzi.
Kiungo 88:11
12
فِيهَا عَيْنٌۭ جَارِيَةٌۭ
Humo imo chemchem inayo miminika. [12]
Maelezo ya chini[12] Humo mna chemchem isiyo katika.
Kiungo 88:12
13
فِيهَا سُرُرٌۭ مَّرْفُوعَةٌۭ
Humo vimo viti vilivyo nyanyuliwa, [13]
Maelezo ya chini[13] Humo vitakuwamo viti vilivyo nyanyuliwa kwa cheo na kwa hakika, kama ni ziada ya neema.
Kiungo 88:13
14
وَأَكْوَابٌۭ مَّوْضُوعَةٌۭ
Na bilauri zilizo pangwa, [14]
Maelezo ya chini[14] Na bilauri (gilasi) zilio wekwa mbele yao,
Kiungo 88:14
15
وَنَمَارِقُ مَصْفُوفَةٌۭ
Na matakia safu safu, [15]
Maelezo ya chini[15] Na mito na matakia yalio pangwa kwa safu.
Kiungo 88:15
16
وَزَرَابِىُّ مَبْثُوثَةٌ
Na mazulia yaliyo tandikwa. [16]
Maelezo ya chini[16] Na mazulia mengi yaliyo tandazwa hapo barazani.
Kiungo 88:16
17
أَفَلَا يَنظُرُونَ إِلَى ٱلْإِبِلِ كَيْفَ خُلِقَتْ
Je! Hawamtazami ngamia jinsi alivyo umbwa? [17]
Maelezo ya chini[17] Je! Wanapuuza kuzingatia Ishara, basi hebu na wamuangalie ngamia, vipi alivyo umbwa kwa namna ya peke yake kwa uweza wa Mwenyezi Mungu? Katika kuumbwa ngamia zipo Ishara na miujiza yenye kuthibitisha uweza wa Mwenyezi Mungu ambao yafaa wenye kuzingatia wauzingatie. Katika sifa zake zinazo onekana ni hizo zinazo mfanya kweli awe ni jahazi ya jangwani. Macho yake yamenyanyuka yako juu ya kichwa, na yanaelekea nyuma, na tena yana kope za kuyakinga na mchanga na vumbi. Kadhaalika pua na masikio yamefunikwa na nywele kwa sababu hiyo hiyo. Ukivuma mdharuba wa mchanga pua hufunga na masikio hupinda, juu ya kuwa tokea hapo ni madogo na si yenye kudhihiri mno, ukilinganisha na mwili wake. Ama miguu ni mirefu kwa kusaidia wepesi wa kwenda, pamoja na kunasibiana na urefu wa shingo yake. Ama nyayo ni pana zimetanda kwa ukhafifu ili kumwezesha ngamia kwenda juu ya mchanga laini. Na ngamia kwa jumla chini ya kifua chake na chini ya viungo vyake vya miguu pana kama mito inayo msaidia ngamia kupiga magoti na kulala juu ya ardhi ngumu na imoto, kama vile vile pande zote mbili za mkia wake yapo manyoya marefu ya kumlinda sehemu zake za nyuma na vitu vya kumuudhi. Ama vipawa alivyo pewa ngamia kwa ajili ya kazi yake ni vya ajabu zaidi. Siku za baridi hahitajii maji, bali anaweza asinywe maji muda wa miezi miwili mfululizo, ikiwa chakula kimajimaji na laini, au wiki mbili ikiwa kikavu. Pia anaweza kustahamili kiu hata siku za joto muda wa wiki au wiki mbili, na hupungua muda huo zaidi ya thuluthi mbili ya uzito wake. Na anapo yapata maji huyagugumia maji kwa wingi mno arejeshe uzito wake wa zamani kwa dakika chache tu. Na ngamia hayarimbiki maji katika tumbo lake kama ilivyo kuwa ikidhaniwa, bali katika mfumo wa mwili wake, na huyatumia kwa uangalifu mkubwa mno. Kwa hivyo kabisa hapumui kama anavyo pumua mbwa, mathalan, wala hatoi pumzi kwa mdomo wake, wala hatoki majasho kwenye ngozi yake ila kwa uchache kabisa. Na hayo ni kuwa daraja ya joto ya mwili wake inakuwa chini sana asubuhi mapema. Kisha hupanda kidogo kidogo zaidi ya daraja sita kabla ya kuhitajia kuipoza kwa jasho na kutoa mvuke. Na juu ya maji mengi mno yanayo toka katika mwili baada ya kiu kirefu kwa hakika uzito wa damu hauathiriki ila kwa kiasi tu, na kwa hivyo kiu hakina athari kitu juu yake. Na imethibiti mafuta ya nunudu yaliyo khaziniwa kwa ajili ya nishat'i yanamkifu kumkinga na machungu ya njaa, lakini hayamfaidishi sana kwa haja ya maji ambayo ni lazima kwa mwili wake. Na bado wataalamu wangali wanagundua mapya katika ngamia kila wakichungua ya kuhakikisha hadhi aliyo mpa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa atazamwe katika uumbaji wake wa muujiza.
Kiungo 88:17
18
وَإِلَى ٱلسَّمَآءِ كَيْفَ رُفِعَتْ
Na mbingu jinsi ilivyo inuliwa? [18]
Maelezo ya chini[18] Na waizingatie mbingu wanayo iona daima, vipi ilivyo nyanyuliwa huko mbali bila ya nguzo!
Kiungo 88:18
19
وَإِلَى ٱلْجِبَالِ كَيْفَ نُصِبَتْ
Na milima jinsi ilivyo thibitishwa? [19]
Maelezo ya chini[19] Na milima wanayo ikwea mpaka wakafika vileleni kwake, vipi ilivyo simamishwa kwa urefu, imeshikamana na ardhi, haiyumbi wala haitikisiki!
Kiungo 88:19
20
وَإِلَى ٱلْأَرْضِ كَيْفَ سُطِحَتْ
Na ardhi jinsi ilivyo tandazwa? [20]
Maelezo ya chini[20] Na ardhi wanayo ikalia na kuyendea juu yake, vipi ilivyo kunjuliwa na kutandazwa! Mara nyingi katika Qur'ani tukufu inatajwa kuwa ardhi "imekunjuliwa". Na makusudio ya hayo ni kuwa ardhi ijapo kuwa ni duara kama mpira kwa sura yake, lakini inavyo onekana kwa watazamao ni kuwa imekunjuliwa. Na haya hayagongani na yaliyo thibitishwa na sayansi katika jambo lolote.
Kiungo 88:20
21
فَذَكِّرْ إِنَّمَآ أَنتَ مُذَكِّرٌۭ
Basi kumbusha! Hakika wewe ni Mkumbushaji. [21]
Maelezo ya chini[21] Basi kumbusha kwa wito wako, kwani kazi yako muhimu ni kufikisha wito tu.
Kiungo 88:21
22
لَّسْتَ عَلَيْهِم بِمُصَيْطِرٍ
Wewe si mwenye kuwatawalia. [22]
Maelezo ya chini[22] Hukuwa mtawala juu yao.
Kiungo 88:22
23
إِلَّا مَن تَوَلَّىٰ وَكَفَرَ
Lakini anaye rudi nyuma na kukataa, [23]
Maelezo ya chini[23] Lakini miongoni mwao ataye puuza na akakataa,
Kiungo 88:23
24
فَيُعَذِّبُهُ ٱللَّهُ ٱلْعَذَابَ ٱلْأَكْبَرَ
Basi Mwenyezi Mungu atamuadhibu kwa adhabu iliyo kubwa kabisa! [24]
Maelezo ya chini[24] Basi Mwenyezi Mungu atampa adhabu iliyo kubwa kabisa, isiyo kuwa na ya kuipita.
Kiungo 88:24
25
إِنَّ إِلَيْنَآ إِيَابَهُمْ
Hakika ni kwetu Sisi ndio marejeo yao. [25]
Maelezo ya chini[25] Hakika ni kwetu Sisi marejeo yao kwa kifo na kufufuliwa, wala hapana penginepo isipo kuwa kwetu.
Kiungo 88:25
26
ثُمَّ إِنَّ عَلَيْنَا حِسَابَهُم
Kisha hakika ni juu yetu Sisi hisabu yao! [26]
Maelezo ya chini[26] Tena ni juu yetu Sisi tu peke yetu kuwahisabia na kuwalipa.
Kiungo 88:26

Soma na usikilize kila siku kwenye programu ya Niyat, pamoja na nyakati za swala, kibla na mahali ulipofikia.

Pata Niyat bure