Sura ya 38 kati ya 114 · Makkiya

Sura Sad

سُورَةُ صٓ
Aya 88

Tafsiri ya maana: Ali Mohsin Al-Barwani, QuranEnc.com, toleo 1.0.1. Tafsiri huwasilisha maana za Qur'ani. Qur'ani yenyewe ni maandishi ya Kiarabu.

بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
1
صٓ ۚ وَٱلْقُرْءَانِ ذِى ٱلذِّكْرِ
S'ad, Naapa kwa Qur'ani yenye mawaidha. [1]
Maelezo ya chini[1] S'ad: Ni harufi iliyo anzia Sura hii kama zilivyo anzia baadhi ya Sura nyengine kwa mpango wa Qur'ani katika kuanzia kwa harufi moja moja. Naapa kwa Qur'ani yenye utukufu na shani kubwa kuwa hakika hii ni Kweli isiyo na shaka yoyote.
Kiungo 38:1
2
بَلِ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ فِى عِزَّةٍۢ وَشِقَاقٍۢ
Lakini walio kufuru wamo katika majivuno na upinzani . [2]
Maelezo ya chini[2] Lakini walio kufuru wamo katika majivuno, hawataki kufuata Haki, na wanawafanyia inda watu wa Haki.
Kiungo 38:2
3
كَمْ أَهْلَكْنَا مِن قَبْلِهِم مِّن قَرْنٍۢ فَنَادَوا۟ وَّلَاتَ حِينَ مَنَاصٍۢ
Mataifa mangapi tumeyaangamiza kabla yao, na wakapiga kelele, lakini wakati wa kuokoka ulikwisha pita. [3]
Maelezo ya chini[3] Mataifa mengi tuliyateketeza kabla yao, wakapiga kelele kutaka msaada ilipo wafikia adhabu. Lakini huo haukuwa wakati wa kuiepuka adhabu.
Kiungo 38:3
4
وَعَجِبُوٓا۟ أَن جَآءَهُم مُّنذِرٌۭ مِّنْهُمْ ۖ وَقَالَ ٱلْكَـٰفِرُونَ هَـٰذَا سَـٰحِرٌۭ كَذَّابٌ
Na walistaajabu kuwajia mwonyaji anaye tokana nao wenyewe, na makafiri wakasema: Huyu ni mchawi, mwongo. [4]
Maelezo ya chini[4] Na walistaajabu watu hawa kuwa amewajia Mtume binaadamu kama wao, na wakasema hao wanao upinga Ujumbe wake: Huyu ni mdanganyifu, mwongo.
Kiungo 38:4
5
أَجَعَلَ ٱلْـَٔالِهَةَ إِلَـٰهًۭا وَٰحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَىْءٌ عُجَابٌۭ
Amewafanya miungu wote kuwa ni Mungu Mmoja tu? Hakika hili ni jambo la ajabu. [5]
Maelezo ya chini[5] Ati amewafanya miungu yote kuwa ni Mungu mmoja tu! Ama hakika jambo hili ni la ajabu, mwisho wa kustaajabisha.
Kiungo 38:5
6
وَٱنطَلَقَ ٱلْمَلَأُ مِنْهُمْ أَنِ ٱمْشُوا۟ وَٱصْبِرُوا۟ عَلَىٰٓ ءَالِهَتِكُمْ ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَىْءٌۭ يُرَادُ
Na wakaondoka wakubwa wao wakiwaambia: Nendeni zenu na dumuni na miungu yenu, kwani hili ni jambo lililo pangwa. [6]
Maelezo ya chini[6] Wakubwa wao wakakimbilia kuusiana wao kwa wao wakiambiana: Endeleeni na njia yenu hiyo hiyo, na shikilieni kuiabudu miungu yenu. Kwani hakika tumepangiwa jambo kubwa hili.
Kiungo 38:6
7
مَا سَمِعْنَا بِهَـٰذَا فِى ٱلْمِلَّةِ ٱلْـَٔاخِرَةِ إِنْ هَـٰذَآ إِلَّا ٱخْتِلَـٰقٌ
Sisi hatukusikia haya katika mila hii ya mwisho. Haya si chochote ila ni uzushi tu. [7]
Maelezo ya chini[7] Hatujapata kusikia haya mambo ya Tawhidi, kumfanya Mungu mmoja tu, katika dini ya baba zetu tulio wawahi kuwaona. Haya si chochote ila ni uwongo tu ulio zuliwa.
Kiungo 38:7
8
أَءُنزِلَ عَلَيْهِ ٱلذِّكْرُ مِنۢ بَيْنِنَا ۚ بَلْ هُمْ فِى شَكٍّۢ مِّن ذِكْرِى ۖ بَل لَّمَّا يَذُوقُوا۟ عَذَابِ
Ati yeye tu ndiye aliye teremshiwa mawaidha peke yake katika sisi? Lakini hao wana shaka na mawaidha yangu, bali hawajaionja adhabu yangu. [8]
Maelezo ya chini[8] Basi katika sote sisi, amechaguliwa Muhammad tu peke yake kupewa hishima ya kuteremshiwa Qur'ani?
Kiungo 38:8
9
أَمْ عِندَهُمْ خَزَآئِنُ رَحْمَةِ رَبِّكَ ٱلْعَزِيزِ ٱلْوَهَّابِ
Au wanazo wao khazina za rehema za Mola wako Mlezi, Mwenye nguvu, Mpaji? [9]
Maelezo ya chini[9] Bali sisi tunawauliza hawa wanao kuhusudu: Kwani wao wanazo khazina za rehema ya Mola wako Mlezi Mwenye nguvu, Mwingi wa kutoa, hata wao wawe ndio wa kuteua nani wa kumpa Unabii kwa mujibu wa mapenzi ya nafsi zao?
Kiungo 38:9
10
أَمْ لَهُم مُّلْكُ ٱلسَّمَـٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا ۖ فَلْيَرْتَقُوا۟ فِى ٱلْأَسْبَـٰبِ
Au wao wana ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo kati yao? Basi nawazipande njia za kwendea huko! [10]
Maelezo ya chini[10] Tena tunawauliza: Kwani wao wanao ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo baina yao? Ikiwa hivyo basi nawazipande ngazi mpaka wafikie pahala ambapo watakuwa wakitoa hukumu kama watakavyo, kama wanaweza!
Kiungo 38:10
11
جُندٌۭ مَّا هُنَالِكَ مَهْزُومٌۭ مِّنَ ٱلْأَحْزَابِ
Hao ni askari watao shindwa miongoni mwa makundi yatayo shindwa. [11]
Maelezo ya chini[11] Hao ni askari wanyonge walio shindwa, hapana hivi wala hivi, kama walivyo shindwa mfano kama wao walio jikusanya kuwapinga Manabii.
Kiungo 38:11
12
كَذَّبَتْ قَبْلَهُمْ قَوْمُ نُوحٍۢ وَعَادٌۭ وَفِرْعَوْنُ ذُو ٱلْأَوْتَادِ
Walikanusha kabla yao kaumu ya Nuhu, na kina A'adi na Firauni mwenye majengo. [12]
Maelezo ya chini[12] Kabla ya hawa, walikadhibisha kaumu ya Nuhu, kina A'adi na Firauni aliye kuwa na majengo makubwa yaliyo simama imara kama milima, na kina Thamudi na Kaumu Lut'i na Kaumu ya Shuaibu, na watu wa Machakani, kwenye miti mingi iliyo shikamana. Hao ndio walio jumuika kuwapinga Mitume wao kama walivyo jumuika watu wako.
Kiungo 38:12
13
وَثَمُودُ وَقَوْمُ لُوطٍۢ وَأَصْحَـٰبُ لْـَٔيْكَةِ ۚ أُو۟لَـٰٓئِكَ ٱلْأَحْزَابُ
Na Thamud na kaumu Lut'i na watu wa Machakani. Hayo ndiyo makundi. [13]
Maelezo ya chini[13] Na kina Thamudi na Kaumu Lut'i na Kaumu ya Shuaibu, na watu wa Machakani, kwenye miti mingi iliyo shikamana. Hao ndio walio jumuika kuwapinga Mitume wao kama walivyo jumuika watu wako.
Kiungo 38:13
14
إِن كُلٌّ إِلَّا كَذَّبَ ٱلرُّسُلَ فَحَقَّ عِقَابِ
Hao wote waliwakadhibisha Mitume; basi wakastahiki adhabu yangu. [14]
Maelezo ya chini[14] Hapana mmoja katika hao wote ila alimkadhibisha Mtume wake, na kwa hivyo ikawashukia adhabu yangu.
Kiungo 38:14
15
وَمَا يَنظُرُ هَـٰٓؤُلَآءِ إِلَّا صَيْحَةًۭ وَٰحِدَةًۭ مَّا لَهَا مِن فَوَاقٍۢ
Na hawa hawangojei ila ukelele mmoja tu usio na muda. [15]
Maelezo ya chini[15] Na hao walio jiunga kuwapinga Mitume hawangojei ila ukelele mmoja usio hitajia kukaririwa.
Kiungo 38:15
16
وَقَالُوا۟ رَبَّنَا عَجِّل لَّنَا قِطَّنَا قَبْلَ يَوْمِ ٱلْحِسَابِ
Na wao husema: Mola wetu Mlezi! Tuletee upesi sehemu yetu ya adhabu kabla ya Siku ya Hisabu. [16]
Maelezo ya chini[16] Na makafiri husema kwa kejeli: Mola wetu Mlezi! Tuhimizie sehemu yetu ya adhabu kabla ya Siku ya Malipo.
Kiungo 38:16
17
ٱصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَٱذْكُرْ عَبْدَنَا دَاوُۥدَ ذَا ٱلْأَيْدِ ۖ إِنَّهُۥٓ أَوَّابٌ
Subiri kwa hayo wayasemayo, na umkumbuke mja wetu Daudi, mwenye nguvu. Hakika yeye alikuwa mwingi wa kutubia. [17]
Maelezo ya chini[17] Ewe Muhammad! Yastahamilie hayo wanayo yasema juu yako washirikina. Na mkumbuke mja wetu, Daudi, mwenye nguvu katika Dini na dunia. Hakika yeye alikuwa mwingi wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu katika hali zote.
Kiungo 38:17
18
إِنَّا سَخَّرْنَا ٱلْجِبَالَ مَعَهُۥ يُسَبِّحْنَ بِٱلْعَشِىِّ وَٱلْإِشْرَاقِ
Hakika tuliidhalilisha milima pamoja naye ikisabihi jioni na asubuhi pamoja naye. [18]
Maelezo ya chini[18] Hakika Sisi tuliidhalilisha milima pamoja naye, yeye akichuma manufaa kutoka humo, na hiyo milima ikimtakasa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kila upungufu, wakati wa mwisho wa mchana na mwanzo wake.
Kiungo 38:18
19
وَٱلطَّيْرَ مَحْشُورَةًۭ ۖ كُلٌّۭ لَّهُۥٓ أَوَّابٌۭ
Na pia ndege walio kusanywa makundi kwa makundi; wote walikuwa wanyenyekevu kwake. [19]
Maelezo ya chini[19] Na pia tukamdhalilishia ndege walio kusanywa kutokana na kila namna na kila pahali. Vyote hivyo, milima na ndege, vikimwitikia Daudi kama atakavyo, akivisarifu kama apendavyo kwa maslaha ya umma.
Kiungo 38:19
20
وَشَدَدْنَا مُلْكَهُۥ وَءَاتَيْنَـٰهُ ٱلْحِكْمَةَ وَفَصْلَ ٱلْخِطَابِ
Na tukautia nguvu ufalme wake, na tukampa hikima, na kukata hukumu. [20]
Maelezo ya chini[20] Tukautia nguvu ufalme wake, na tukampa Unabii na kupambanua baina ya Haki na baat'ili.
Kiungo 38:20
21
۞ وَهَلْ أَتَىٰكَ نَبَؤُا۟ ٱلْخَصْمِ إِذْ تَسَوَّرُوا۟ ٱلْمِحْرَابَ
Na je! Imekufikia khabari ya wagombanao walipo pindukia ukuta kuingia chumbani? [21]
Maelezo ya chini[21] Ewe Muhammad! Ati imekujia khabari ya makhasimu wagombanao, walio mjia Daudi kwa kupindukia kuta za mihrabuni palipo kuwa pahala pake pa ibada? Hawakupita mlangoni.
Kiungo 38:21
22
إِذْ دَخَلُوا۟ عَلَىٰ دَاوُۥدَ فَفَزِعَ مِنْهُمْ ۖ قَالُوا۟ لَا تَخَفْ ۖ خَصْمَانِ بَغَىٰ بَعْضُنَا عَلَىٰ بَعْضٍۢ فَٱحْكُم بَيْنَنَا بِٱلْحَقِّ وَلَا تُشْطِطْ وَٱهْدِنَآ إِلَىٰ سَوَآءِ ٱلصِّرَٰطِ
Walipo muingilia Daudi, naye akawaogopa. Wakasema: Usiogope! Sisi ni wagombanao wawili, mmoja wetu amemdhulumu mwenziwe. Basi tuhukumu kwa haki, wala usipendelee. Na utuongoe kwenye njia iliyo sawa. [22]
Maelezo ya chini[22] Walipo muingilia Daudi, naye akawaogopa, akababaika. Wakasema: Usikhofu kitu. Sisi ni wenye kuzozana, tumedhulumiana. Basi tuhukumu kwa uadilifu wala usiupindukie huo uadilifu. Na tuongoze kwenye njia iliyo sawa sawa.
Kiungo 38:22
23
إِنَّ هَـٰذَآ أَخِى لَهُۥ تِسْعٌۭ وَتِسْعُونَ نَعْجَةًۭ وَلِىَ نَعْجَةٌۭ وَٰحِدَةٌۭ فَقَالَ أَكْفِلْنِيهَا وَعَزَّنِى فِى ٱلْخِطَابِ
Hakika huyu ndugu yangu ana kondoo wa kike tisiini na tisa; na mimi ninaye kondoo mke mmoja. Akasema: Nipe huyo nikufugie! Na amenishinda kwa maneno. [23]
Maelezo ya chini[23] Mmoja wa hao wagombanao alisema: Hakika huyu ndugu yangu anao kondoo wa kike tisiini na tisa, na mimi ninaye kondoo mmoja tu. Akasema: Nache niwe nakuchungia kama ninavyo wachunga wangu. Na akanishinda katika usemi.
Kiungo 38:23
24
قَالَ لَقَدْ ظَلَمَكَ بِسُؤَالِ نَعْجَتِكَ إِلَىٰ نِعَاجِهِۦ ۖ وَإِنَّ كَثِيرًۭا مِّنَ ٱلْخُلَطَآءِ لَيَبْغِى بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ إِلَّا ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ وَعَمِلُوا۟ ٱلصَّـٰلِحَـٰتِ وَقَلِيلٌۭ مَّا هُمْ ۗ وَظَنَّ دَاوُۥدُ أَنَّمَا فَتَنَّـٰهُ فَٱسْتَغْفَرَ رَبَّهُۥ وَخَرَّ رَاكِعًۭا وَأَنَابَ ۩
Akasema: Kweli amekudhulumu kwa kumtaka kondoo wako mmoja kuongezea kwenye kondoo wake. Na hakika washirika wengi hudhulumiana wao kwa wao, isipo kuwa walio amini na wakatenda mema. Na hao ni wachache. Na Daudi akajua kuwa tumemfanyia mtihani. Basi akamwomba msamaha Mola wake Mlezi, na akaanguka kusujudu na kutubia. [24]
Maelezo ya chini[24] Daudi akasema kabla hajasikia maneno ya yule mwenye ugomvi mwengine: Hakika huyo amekudhulumu kwa kumtaka kondoo wako amchanganye na wale wake. Na hakika wengi wenye kushirikiana hudhulumiana wao kwa wao, isipo kuwa wale ambao Imani yao imetulia katika nyoyo zao, na wakawa wanatenda mema. Na watu kama hao ni wachache, shida kupatikana. Na Daudi akajua kuwa jambo hili si chochote ila ni mtihani tuliyo mfanyia Sisi. Basi akaomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu, na akainama kurukuu kwa Mwenyezi Mungu, na akarejea kwa Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu.
Kiungo 38:24
25
فَغَفَرْنَا لَهُۥ ذَٰلِكَ ۖ وَإِنَّ لَهُۥ عِندَنَا لَزُلْفَىٰ وَحُسْنَ مَـَٔابٍۢ
Basi tukamsamehe kwa hayo. Naye kwa hakika anao mkaribisho mkubwa na marejeo mazuri kwetu. [25]
Maelezo ya chini[25] Na Sisi tukamsamehe kule kufanya haraka ya kutoa hukumu. Na hali yeye ana hadhi na marejeo mazuri kwetu.
Kiungo 38:25
26
يَـٰدَاوُۥدُ إِنَّا جَعَلْنَـٰكَ خَلِيفَةًۭ فِى ٱلْأَرْضِ فَٱحْكُم بَيْنَ ٱلنَّاسِ بِٱلْحَقِّ وَلَا تَتَّبِعِ ٱلْهَوَىٰ فَيُضِلَّكَ عَن سَبِيلِ ٱللَّهِ ۚ إِنَّ ٱلَّذِينَ يَضِلُّونَ عَن سَبِيلِ ٱللَّهِ لَهُمْ عَذَابٌۭ شَدِيدٌۢ بِمَا نَسُوا۟ يَوْمَ ٱلْحِسَابِ
Ewe Daudi! Hakika Sisi tumekufanya wewe uwe Khalifa katika nchi. Basi wahukumu watu kwa haki, wala usifuate matamanio yakakupoteza kwenye Njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika wanao ipotea Njia ya Mwenyezi Mungu wakaiacha, watapata adhabu kali kwa sababu ya kusahau kwao Siku ya Hisabu. [26]
Maelezo ya chini[26] Na Mwenyezi Mungu alimfunulia kwa kumwambia: Ewe Daudi! Hakika Sisi tumekufanya wewe uwe Khalifa, yaani Naibu, wetu katika ardhi. Basi wahukumu watu kwa sharia niliyo kupa, wala usiendeshe hukumu kufuata matamanio yao, yakakupotosha njia ya Mwenyezi Mungu. Hakika wendao pogo na njia ya Mwenyezi Mungu kwa kufuata matamanio yao wao watapata adhabu kali kwa kughafilika kwao na Siku ya Malipo.
Kiungo 38:26
27
وَمَا خَلَقْنَا ٱلسَّمَآءَ وَٱلْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا بَـٰطِلًۭا ۚ ذَٰلِكَ ظَنُّ ٱلَّذِينَ كَفَرُوا۟ ۚ فَوَيْلٌۭ لِّلَّذِينَ كَفَرُوا۟ مِنَ ٱلنَّارِ
Na hatukuziumba mbingu na ardhi na viliomo ndani yao bure. Hiyo ni dhana ya walio kufuru. Ole wao walio kufuru kwa Moto utao wapata. [27]
Maelezo ya chini[27] Wala Sisi hatukuziumba mbingu na ardhi na viliomo baina yao kwa mchezo. Hayo ndiyo wanayo yadhania makafiri. Na kwa hivyo wakapitisha hukumu kwa mujibu wa pumbao zao. Basi hao walio kufuru watapata adhabu kali ya Moto.
Kiungo 38:27
28
أَمْ نَجْعَلُ ٱلَّذِينَ ءَامَنُوا۟ وَعَمِلُوا۟ ٱلصَّـٰلِحَـٰتِ كَٱلْمُفْسِدِينَ فِى ٱلْأَرْضِ أَمْ نَجْعَلُ ٱلْمُتَّقِينَ كَٱلْفُجَّارِ
Je! Tuwafanye walio amini na wakatenda mema kama wafanyao uharibifu katika nchi? Au tuwafanye wachamngu kama waovu? [28]
Maelezo ya chini[28] Inaelekeana vipi na hikima yetu na uadilifu wetu tuwafanye sawa baina ya Waumini wenye kutenda mema, na wale wanao fanya uharibifu katika ardhi? Au yaelekea vipi tuwaweke sawa baina ya wenye kuikhofu adhabu yetu na wakaiogopa ikabu yetu na wale walio waasi wakenda kinyume na hukumu zetu?
Kiungo 38:28
29
كِتَـٰبٌ أَنزَلْنَـٰهُ إِلَيْكَ مُبَـٰرَكٌۭ لِّيَدَّبَّرُوٓا۟ ءَايَـٰتِهِۦ وَلِيَتَذَكَّرَ أُو۟لُوا۟ ٱلْأَلْبَـٰبِ
Na hiki Kitabu, tumekuteremshia wewe, kimebarikiwa, ili wazizingatie Aya zake, na wawaidhike wenye akili. [29]
Maelezo ya chini[29] Ewe Muhammad! Hichi tulicho kuteremshia ni Kitabu chenye manufaa mengi, ili wenye akili nzuri na nyoyo za kufahamu wapate kuzielewa Aya zake, na wawaidhike kwazo.
Kiungo 38:29
30
وَوَهَبْنَا لِدَاوُۥدَ سُلَيْمَـٰنَ ۚ نِعْمَ ٱلْعَبْدُ ۖ إِنَّهُۥٓ أَوَّابٌ
Na Daudi tukamtunukia Suleiman. Alikuwa mja mwema. Na hakika alikuwa mwingi wa kutubia. [30]
Maelezo ya chini[30] Na Daudi tulimtunukia mwana, aitwaye Suleiman, mwenye kustahiki sifa nzuri, ambaye anafaa kuitwa, "Mja mwema kweli". Kwa sababu yeye alikuwa mwingi mno wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu katika kila hali.
Kiungo 38:30
31
إِذْ عُرِضَ عَلَيْهِ بِٱلْعَشِىِّ ٱلصَّـٰفِنَـٰتُ ٱلْجِيَادُ
Alipo pelekewa jioni farasi wasimamao kidete, tayari kutoka shoti; [31]
Maelezo ya chini[31] Na hebu taja katika khabari za Suleiman kuwa alipelekewa alasiri farasi wa asli ambao hutulia wanapo simama, na huenda mbio wanapo kwenda.
Kiungo 38:31
32
فَقَالَ إِنِّىٓ أَحْبَبْتُ حُبَّ ٱلْخَيْرِ عَن ذِكْرِ رَبِّى حَتَّىٰ تَوَارَتْ بِٱلْحِجَابِ
Basi akasema: Navipenda vitu vizuri kwa kumkumbuka Mola wangu Mlezi. Kisha wakafichikana nyuma ya boma. [32]
Maelezo ya chini[32] Suleiman akasema: Hakika mimi nimenyweshwa mapenzi ya farasi, kwa sababu hawa ni katika matayarisho ya mambo ya kheri, nayo ni Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Mapenzi haya yametokana na kumkumbuka Mola wangu Mlezi. Na hakusita kushughulika kuwaangalia mpaka wakapotea machoni mwake.
Kiungo 38:32
33
رُدُّوهَا عَلَىَّ ۖ فَطَفِقَ مَسْحًۢا بِٱلسُّوقِ وَٱلْأَعْنَاقِ
Nirudishieni! Akaanza kuwapapasa miguu na shingo. [33]
Maelezo ya chini[33] Akaamrisha warudishwe tena kwake apate kujua hali yao. Akaingia kuwapapasa miundi ya miguu yao na shingo zao kwa upole na mapenzi juu yao.
Kiungo 38:33
34
وَلَقَدْ فَتَنَّا سُلَيْمَـٰنَ وَأَلْقَيْنَا عَلَىٰ كُرْسِيِّهِۦ جَسَدًۭا ثُمَّ أَنَابَ
Na tulimtia mtihanini Suleiman, na tukauweka mwili juu ya kiti chake, kisha akarejea kwa kutubu. [34]
Maelezo ya chini[34] Na hakika Sisi tulimfanyia mtihani Suleiman ili asighurike na heba ya ufalme. Tukaweka juu ya kiti chake kiwiliwili kisicho weza kuendesha mambo. Akautambua mtihani, akarejea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na akatubu.
Kiungo 38:34
35
قَالَ رَبِّ ٱغْفِرْ لِى وَهَبْ لِى مُلْكًۭا لَّا يَنۢبَغِى لِأَحَدٍۢ مِّنۢ بَعْدِىٓ ۖ إِنَّكَ أَنتَ ٱلْوَهَّابُ
Akasema: Mola wangu Mlezi! Nisamehe na unipe ufalme usio mwelekea yeyote baada yangu. Hakika Wewe ndiye Mpaji. [35]
Maelezo ya chini[35] Suleiman alimwomba Mola wake Mlezi kwa kurejea kwake: Mola wangu Mlezi! Nighufirie yaliyo toka kwangu kwa ghafla, na unitunukie ufalme usio elekea yeyote kuupata baada yangu. Hakika Wewe ndiye Mwingi wa kutunukia, na ndiye Mwingi wa kutoa.
Kiungo 38:35
36
فَسَخَّرْنَا لَهُ ٱلرِّيحَ تَجْرِى بِأَمْرِهِۦ رُخَآءً حَيْثُ أَصَابَ
Basi tukaufanya upepo umtumikie, ukenda kwa amri yake, popote alipo taka kufika. [36]
Maelezo ya chini[36] Tukamdhalilishia upepo, ukenda kama anavyo taka maridhawa, kokote aliko kusudia na kutaka.
Kiungo 38:36
37
وَٱلشَّيَـٰطِينَ كُلَّ بَنَّآءٍۢ وَغَوَّاصٍۢ
Na tukayafanya mashet'ani yamtumikie, wote wajenzi na wapiga mbizi. [37]
Maelezo ya chini[37] Na tukamdhalilishia kila mjenzi na mpiga mbizi katika bahari kuu miongoni mwa mashetani maasi.
Kiungo 38:37
38
وَءَاخَرِينَ مُقَرَّنِينَ فِى ٱلْأَصْفَادِ
Na wengine wafungwao kwa minyororo. [38]
Maelezo ya chini[38] Na wengine katika hao mashetani wamefungwa wao kwa wao kwa minyororo, kuwazuia na wenginewe wasifanye ufisadi wao.
Kiungo 38:38
39
هَـٰذَا عَطَآؤُنَا فَٱمْنُنْ أَوْ أَمْسِكْ بِغَيْرِ حِسَابٍۢ
Hichi ndicho kipawa chetu. Basi toa au zuia, bila ya hisabu. [39]
Maelezo ya chini[39] Na akamfunulia kwa wahyi : Haya tuliyo kuneemesha kwayo ni kipawa kilicho toka kwetu. Yaani ni Sisi tulio kupa. Basi mpe umtakaye, na mnyime umtakaye. Hapana hisabu juu yako kwa kutoa au kunyima.
Kiungo 38:39
40
وَإِنَّ لَهُۥ عِندَنَا لَزُلْفَىٰ وَحُسْنَ مَـَٔابٍۢ
Na hakika yeye kwetu Sisi ana cheo cha kukaribishwa kwetu, na pahala pazuri pa kurejea. [40]
Maelezo ya chini[40] Hakika Suleiman kwetu Sisi ana ukaribisho mkubwa, na marejeo mazuri.
Kiungo 38:40
41
وَٱذْكُرْ عَبْدَنَآ أَيُّوبَ إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُۥٓ أَنِّى مَسَّنِىَ ٱلشَّيْطَـٰنُ بِنُصْبٍۢ وَعَذَابٍ
Na mkumbuke mja wetu Ayubu alipo mwita Mola wake Mlezi akasema: Kwa hakika Shet'ani amenifikishia udhia na adhabu. [41]
Maelezo ya chini[41] Ewe Muhammad! Mkumbuke mja wetu Ayubu alipo mwomba Mola wake Mlezi kwa kusema: Hakika Shetani amenipatisha taabu na machungu.
Kiungo 38:41
42
ٱرْكُضْ بِرِجْلِكَ ۖ هَـٰذَا مُغْتَسَلٌۢ بَارِدٌۭ وَشَرَابٌۭ
(Akaambiwa:) Piga-piga ardhi kwa mguu wako! Basi haya maji baridi ya kuogea na ya kunywa. [42]
Maelezo ya chini[42] Tukamuitikia na tukamwambia: Ipige ardhi kwa mguu wako, yatatimbuka maji baridi, utakoga na utakunywa hayo, na kwa hivyo yatakuondokea machofu na adhabu.
Kiungo 38:42
43
وَوَهَبْنَا لَهُۥٓ أَهْلَهُۥ وَمِثْلَهُم مَّعَهُمْ رَحْمَةًۭ مِّنَّا وَذِكْرَىٰ لِأُو۟لِى ٱلْأَلْبَـٰبِ
Na tukampa ahali zake na wengine kama wao pamoja nao, kuwa ni rehema itokayo kwetu, na iwe kumbusho kwa watu wenye akili. [43]
Maelezo ya chini[43] Tukamkusanyia watu wake walio kuwa wametapanyika mbali naye siku zile za mateso yake. Na tukamzidishia wenginewe kama wale. Na tulifanya hayo kuwa ni rehema kutokana nasi, na ili yawe ni mawaidha kwa wenye akili, wapate kujua kuwa matokeo ya subira ni faraji.
Kiungo 38:43
44
وَخُذْ بِيَدِكَ ضِغْثًۭا فَٱضْرِب بِّهِۦ وَلَا تَحْنَثْ ۗ إِنَّا وَجَدْنَـٰهُ صَابِرًۭا ۚ نِّعْمَ ٱلْعَبْدُ ۖ إِنَّهُۥٓ أَوَّابٌۭ
Na shika kicha cha vijiti tu mkononi mwako, kisha ndio upigie nacho, wala usivunje kiapo. Hakika tulimkuta mwenye subira, mbora wa waja, kwa hakika alikuwa mwingi wa kutubu. [44]
Maelezo ya chini[44] Ayubu alikuwa kaapa kuwa atampiga mmoja wapo katika ahali zake fimbo kadhaa wa kadhaa. Mwenyezi Mungu alimhalalishia aondoe kiapo chake kwa kuchukua kifungu cha fimbo idadi ile ile alio apia kuwa atampigia. Basi kwa kile kifungu cha fimbo ampige aliye apa kuwa atampiga, na hapo yamini yake itakuwa imetimia kwa uchache wa machungu. Mwenyezi Mungu ndiye aliye mneemesha kwa neema hizi, kwa sababu Mwenyezi Mungu alimwona kuwa ni mtu aliye vumilia masaibu yake. Kwa hivyo amestahiki sifa. Mbora wa kusifiwa kwa ibada ni yeye, kwa sababu yeye ni mwingi mno wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu katika kila jambo.
Kiungo 38:44
45
وَٱذْكُرْ عِبَـٰدَنَآ إِبْرَٰهِيمَ وَإِسْحَـٰقَ وَيَعْقُوبَ أُو۟لِى ٱلْأَيْدِى وَٱلْأَبْصَـٰرِ
Na wakumbuke waja wetu, Ibrahim na Is-haqa na Yaa'qubu walio kuwa na nguvu na busara. [45]
Maelezo ya chini[45] Na mkumbuke mja wetu Ibrahim, na Is-haqa, na Yaa'qubu, wenye nguvu katika Dini na dunia, na wenye busara ya mwangaza.
Kiungo 38:45
46
إِنَّآ أَخْلَصْنَـٰهُم بِخَالِصَةٍۢ ذِكْرَى ٱلدَّارِ
Sisi tumewakhusisha wao kwa sifa ya ukumbusho wa Akhera. [46]
Maelezo ya chini[46] Hakika Sisi tumewakhusisha wao kwa sifa, nayo ni kuwa wanaikumbuka Nyumba ya Akhera, wao wanaikumbuka nao wanakumbukwa kwayo.
Kiungo 38:46
47
وَإِنَّهُمْ عِندَنَا لَمِنَ ٱلْمُصْطَفَيْنَ ٱلْأَخْيَارِ
Na hakika wao kwetu sisi ni wateuliwa walio bora. [47]
Maelezo ya chini[47] Na hakika wao kwetu Sisi ni wenye kukhitariwa walio bora.
Kiungo 38:47
48
وَٱذْكُرْ إِسْمَـٰعِيلَ وَٱلْيَسَعَ وَذَا ٱلْكِفْلِ ۖ وَكُلٌّۭ مِّنَ ٱلْأَخْيَارِ
Na mkumbuke Ismail na Alyasaa na Dhulkifli, na wote hao ni katika walio bora. [48]
Maelezo ya chini[48] Na mkumbuke Ismail, na Alyasaa, na Dhalkifli - na wote hao ni miongoni mwa walio bora.
Kiungo 38:48
49
هَـٰذَا ذِكْرٌۭ ۚ وَإِنَّ لِلْمُتَّقِينَ لَحُسْنَ مَـَٔابٍۢ
Huu ni ukumbusho. Na hakika wachamngu wana marudio mazuri. [49]
Maelezo ya chini[49] Haya tuliyo kusimulia ni khabari za baadhi ya Mitume ili kukukumbusha wewe na kuwakumbusha watu wako. Na hakika wachamngu walio jikinga na kumuasi Mwenyezi Mungu Mtukufu watapata marejeo mazuri na natija njema.
Kiungo 38:49
50
جَنَّـٰتِ عَدْنٍۢ مُّفَتَّحَةًۭ لَّهُمُ ٱلْأَبْوَٰبُ
Bustani za milele zitazo funguliwa milango yao kwa ajili yao. [50]
Maelezo ya chini[50] Wameandaliwa bustani za milele zilizo funguliwa milango yao hapana wa kuwazuia wasiingie humo.
Kiungo 38:50
51
مُتَّكِـِٔينَ فِيهَا يَدْعُونَ فِيهَا بِفَـٰكِهَةٍۢ كَثِيرَةٍۢ وَشَرَابٍۢ
Humo wataegemea matakia, wawe wanaagiza humo matunda mengi na vinywaji. [51]
Maelezo ya chini[51] Watakuwa wamekaa humo wakiegemea juu ya makochi na vitanda kama wafanyavyo wenye taanusi, wakistarehe kwa kutaka matunda ya kila namna na vinywaji.
Kiungo 38:51
52
۞ وَعِندَهُمْ قَـٰصِرَٰتُ ٱلطَّرْفِ أَتْرَابٌ
Na pamoja nao wake zao wenye kutuliza macho, hirimu zao. [52]
Maelezo ya chini[52] Na huko Peponi watakuwa na wake ambao macho yao hayawatazami ila waume zao tu, hawawaangalii wengineo, nao ni wa miaka sawa na waume zao. Kwa hivyo wameelekeana kuwafikiana.
Kiungo 38:52
53
هَـٰذَا مَا تُوعَدُونَ لِيَوْمِ ٱلْحِسَابِ
aya ndiyo mliyo ahidiwa kwa Siku ya Hisabu. [53]
Maelezo ya chini[53] Raha hii ndiyo mliyo ahidiwa kuipata Siku ya Kiyama.
Kiungo 38:53
54
إِنَّ هَـٰذَا لَرِزْقُنَا مَا لَهُۥ مِن نَّفَادٍ
Hakika hii ndiyo riziki yetu isiyo malizika. [54]
Maelezo ya chini[54] Hakika haya bila ya shaka ni tunayo yatoa Sisi, na wala hayana ukomo.
Kiungo 38:54
55
هَـٰذَا ۚ وَإِنَّ لِلطَّـٰغِينَ لَشَرَّ مَـَٔابٍۢ
Ndio hivi! Na hakika wenye kuasi bila ya shaka watapata marudio maovu kabisa; [55]
Maelezo ya chini[55] Neema hizi ni malipo ya wachamngu. Na hakika majabari wenye kuwaasi Manabii wao bila ya shaka watakuwa na marejeo na mwisho muovu.
Kiungo 38:55
56
جَهَنَّمَ يَصْلَوْنَهَا فَبِئْسَ ٱلْمِهَادُ
Nayo ni Jahannamu! Wataingia humo. Nacho hicho ni kitanda kiovu mno cha kulalia. [56]
Maelezo ya chini[56] Na mwisho huo ni Jahannamu watakayo iingia, na moto wake uwatese. Na malalio maovu mno hayo!
Kiungo 38:56
57
هَـٰذَا فَلْيَذُوقُوهُ حَمِيمٌۭ وَغَسَّاقٌۭ
Ndio hivi! Basi na wayaonje maji ya moto na ya usaha! [57]
Maelezo ya chini[57] Haya maji ya moto, mwisho wa umoto, na usaha wa watu wa Jahannamu wataamrishwa wayaonje.
Kiungo 38:57
58
وَءَاخَرُ مِن شَكْلِهِۦٓ أَزْوَٰجٌ
Na adhabu nyenginezo za namna hii. [58]
Maelezo ya chini[58] Na adhabu nyengine mfano wa hizi, za namna kwa namna zilizo changanyika.
Kiungo 38:58
59
هَـٰذَا فَوْجٌۭ مُّقْتَحِمٌۭ مَّعَكُمْ ۖ لَا مَرْحَبًۢا بِهِمْ ۚ إِنَّهُمْ صَالُوا۟ ٱلنَّارِ
Hili ndilo kundi litakalo ingia pamoja nanyi. Hapana makaribisho mema kwao. Hakika hao wanaingia Motoni. [59]
Maelezo ya chini[59] Na majabari, wale marais wa washirikina, wataambiwa: Hawa chungu ya watu wanao ingia Motoni pamoja nanyi kwa kusukumana na kwa shida, ni wafwasi wenu. Wale marais watasema: Hawana mapokezi mema hao! Hakika hao wanaingia Motoni wapate kuteseka kwa mvukuto wake.
Kiungo 38:59
60
قَالُوا۟ بَلْ أَنتُمْ لَا مَرْحَبًۢا بِكُمْ ۖ أَنتُمْ قَدَّمْتُمُوهُ لَنَا ۖ فَبِئْسَ ٱلْقَرَارُ
Waseme: Lakini nyinyi! Hamna mapokezi mazuri! Nyinyi ndio mlio tusabibisha haya, napo ni pahala paovu kabisa! [60]
Maelezo ya chini[60] Na wafwasi hao watasema: Bali nyinyi ndio mnastahiki zaidi hayo maapizo mnayo tuapizia sisi, kwani nyinyi ndio mlio tuletea adhabu hii kwa vile mlivyo tudanganya na mkatuitia ukafirini, nasi tukakufuru kwa sababu yenu. Basi nyumba ovu kabisa ya kukaa ni Jahannamu!
Kiungo 38:60
61
قَالُوا۟ رَبَّنَا مَن قَدَّمَ لَنَا هَـٰذَا فَزِدْهُ عَذَابًۭا ضِعْفًۭا فِى ٱلنَّارِ
Waseme: Mola wetu Mlezi! Aliye tusabibisha haya mzidishie adhabu mara mbili Motoni. [61]
Maelezo ya chini[61] Wafwasi watasema: Ewe Mola wetu Mlezi! Aliye kuwa ni sababu ya adhabu hii, mzidishie adhabu mara mbili katika Moto.
Kiungo 38:61
62
وَقَالُوا۟ مَا لَنَا لَا نَرَىٰ رِجَالًۭا كُنَّا نَعُدُّهُم مِّنَ ٱلْأَشْرَارِ
Watasema: Tuna nini hata hatuwaoni wale watu ambao tukiwahisabu ndio katika waovu? [62]
Maelezo ya chini[62] Na watu wa Motoni watasema: Mbona hatuwaoni wale watu ambao tulikuwa duniani tukiwahisabu kuwa ndio katika waovu, na wa duni, wasio kuwa na jema lolote? Na watu hao ni wale mafakiri wa Kiislamu.
Kiungo 38:62
63
أَتَّخَذْنَـٰهُمْ سِخْرِيًّا أَمْ زَاغَتْ عَنْهُمُ ٱلْأَبْصَـٰرُ
Tulikosea tulipo wafanyia maskhara, au macho yetu tu hayawaoni ? [63]
Maelezo ya chini[63] Imekuwaje kuwa sisi tukiwakejeli na wala hawakuingia Motoni pamoja nasi? Au wamekwisha ingia na macho yetu yakazibwa tusiwaone tu?
Kiungo 38:63
64
إِنَّ ذَٰلِكَ لَحَقٌّۭ تَخَاصُمُ أَهْلِ ٱلنَّارِ
Hakika hayo bila ya shaka ndiyo makhasimiano ya watu wa Motoni. [64]
Maelezo ya chini[64] Hakika hayo tuliyo yataja ya hadithi ya watu wa Motoni ni kweli ambayo haina budi kutokea, nayo ni ya kugombana kwa watu wa Motoni wao kwa wao.
Kiungo 38:64
65
قُلْ إِنَّمَآ أَنَا۠ مُنذِرٌۭ ۖ وَمَا مِنْ إِلَـٰهٍ إِلَّا ٱللَّهُ ٱلْوَٰحِدُ ٱلْقَهَّارُ
Sema: Hakika mimi ni mwonyaji tu; na hapana mungu ila Mwenyezi Mungu Mmoja, Mtenda nguvu, [65]
Maelezo ya chini[65] Ewe Muhammad! Waambie washirikina: Hakika mimi ni mwenye kukuonyeni na adhabu ya Mwenyezi Mungu, na hapana wa kuabudiwa kwa haki ila Mwenyezi Mungu Mmoja ambaye hana mshirika wake, Mtenda nguvu, Mwenye kumshinda kila mwenye madaraka.
Kiungo 38:65
66
رَبُّ ٱلسَّمَـٰوَٰتِ وَٱلْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا ٱلْعَزِيزُ ٱلْغَفَّـٰرُ
Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na viliomo baina yake, Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe. [66]
Maelezo ya chini[66] Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na viliomo baina yao, Mwenye nguvu asiye shindika, Mwenye kusamehe, akazifuta dhambi za mwenye kumuamini.
Kiungo 38:66
67
قُلْ هُوَ نَبَؤٌا۟ عَظِيمٌ
Sema: Hii ni khabari kubwa kabisa. [67]
Maelezo ya chini[67] Ewe Muhammad! Waambie: Haya ninayo kuambieni ni khabari kubwa, ambazo nyinyi mnazipuuza. Msizikanye!
Kiungo 38:67
68
أَنتُمْ عَنْهُ مُعْرِضُونَ
Ambayo nyinyi mnaipuuza. [68]
Maelezo ya chini[68] Ewe Muhammad! Waambie: Haya ninayo kuambieni ni khabari kubwa, ambazo nyinyi mnazipuuza. Msizikanye!
Kiungo 38:68
69
مَا كَانَ لِىَ مِنْ عِلْمٍۭ بِٱلْمَلَإِ ٱلْأَعْلَىٰٓ إِذْ يَخْتَصِمُونَ
Sikuwa na ilimu ya mambo ya viumbe wakuu watukufu walipo kuwa wakishindana. [69]
Maelezo ya chini[69] Mimi sikuwa nikijua khabari za watukufu walio juu walipo kuwa wakizozana juu ya shauri ya Adam, kwa sababu mimi sikupitia njia za kupata ilimu zilizo zowewa na watu za kusoma vitabu au kupokea masomo kwa wataalamu. Njia yangu mimi ya kujua ni kwa kufunuliwa kwa Wahyi.
Kiungo 38:69
70
إِن يُوحَىٰٓ إِلَىَّ إِلَّآ أَنَّمَآ أَنَا۠ نَذِيرٌۭ مُّبِينٌ
Haikufunuliwa kwangu isipo kuwa ya kwamba hakika mimi ni mwonyaji dhaahiri. [70]
Maelezo ya chini[70] Na mimi sikufunuliwa kwa Wahyi ila kwamba hakika mimi ni Mtume wa kukufikishieni Ujumbe wa Mola wangu Mlezi kwa njia iliyo wazi kabisa.
Kiungo 38:70
71
إِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلَـٰٓئِكَةِ إِنِّى خَـٰلِقٌۢ بَشَرًۭا مِّن طِينٍۢ
Mola wako Mlezi alipo waambia Malaika: Hakika Mimi nitaumba mtu kutokana na udongo. [71]
Maelezo ya chini[71] Watajie pale alipo sema Mola wako Mlezi kuwaambia Malaika: Mimi nataka umba mtu, naye ni Adam a.s., kutokana na udongo.
Kiungo 38:71
72
فَإِذَا سَوَّيْتُهُۥ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِن رُّوحِى فَقَعُوا۟ لَهُۥ سَـٰجِدِينَ
Na nitakapo mkamilisha na kumpulizia roho inayo tokana nami, basi muangukieni kwa kumt'ii. [72]
Maelezo ya chini[72] Nikisha timiza kumuumba na nikampulizia siri ya uhai, nayo ni roho, muangukieni kwa kusujudu sijida ya kumtukuza na kumuamkia.
Kiungo 38:72
73
فَسَجَدَ ٱلْمَلَـٰٓئِكَةُ كُلُّهُمْ أَجْمَعُونَ
Basi Malaika wakat'ii wote pamoja. [73]
Maelezo ya chini[73] Malaika wote wakafanya kama walivyo amrishwa, wakamuangukia wakisujudu, isipo kuwa Iblisi. Yeye hakusujudu, na akajiona bora na akapanda kiburi, na akawa miongoni mwa makafiri.
Kiungo 38:73
74
إِلَّآ إِبْلِيسَ ٱسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ ٱلْكَـٰفِرِينَ
Isipo kuwa Iblisi; alijivuna na akawa katika makafiri. [74]
Maelezo ya chini[74] Malaika wote wakafanya kama walivyo amrishwa, wakamuangukia wakisujudu, isipo kuwa Iblisi. Yeye hakusujudu, na akajiona bora na akapanda kiburi, na akawa miongoni mwa makafiri.
Kiungo 38:74
75
قَالَ يَـٰٓإِبْلِيسُ مَا مَنَعَكَ أَن تَسْجُدَ لِمَا خَلَقْتُ بِيَدَىَّ ۖ أَسْتَكْبَرْتَ أَمْ كُنتَ مِنَ ٱلْعَالِينَ
Mwenyezi Mungu akamwambia: Ewe Iblisi! Kipi kilicho kuzuia kumt'ii yule niliye muumba kwa mikono yangu? Je! Umejiona mkubwa, au umekuwa katika wakuu kweli? [75]
Maelezo ya chini[75] Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema: Ewe Iblisi! Nini kilicho kuzuilia kumsujudia niliye muumba Mimi mwenyewe bila ya kuingiliwa na yeyote kati yake! Umejiona mkubwa hali nawe si mkubwa, au hakika wewe nafsi yako ni katika walio shinda ukubwa?
Kiungo 38:75
76
قَالَ أَنَا۠ خَيْرٌۭ مِّنْهُ ۖ خَلَقْتَنِى مِن نَّارٍۢ وَخَلَقْتَهُۥ مِن طِينٍۢ
Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, na yeye umemuumba kwa udongo. [76]
Maelezo ya chini[76] Iblisi akasema: Mimi ni bora kuliko Adam; kwani Wewe umeniumba kwa moto, na yeye umemuumba kwa udongo. Basi vipi mimi nimsujudie yeye?
Kiungo 38:76
77
قَالَ فَٱخْرُجْ مِنْهَا فَإِنَّكَ رَجِيمٌۭ
Akasema: Basi toka humo, kwani hakika wewe umelaanika. [77]
Maelezo ya chini[77] Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa kumlipa Iblisi kwa kiburi chake cha kukataa amri ya Mola wake Mlezi, alimwambia: Basi toka kwenye kundi la watukufu walio juu, kwani wewe umekwisha fukuzwa kutokana na rehema yangu!
Kiungo 38:77
78
وَإِنَّ عَلَيْكَ لَعْنَتِىٓ إِلَىٰ يَوْمِ ٱلدِّينِ
Na hakika laana yangu itakuwa juu yako mpaka Siku ya Malipo. [78]
Maelezo ya chini[78] Na hakika wewe umetengwa mbali na kila kheri mpaka Siku ya Malipo. Hapo utalipwa kwa sababu ya kunikufuru Mimi na kunifanyia kiburi.
Kiungo 38:78
79
قَالَ رَبِّ فَأَنظِرْنِىٓ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ
Akasema: Mola wangu Mlezi! Nipe muhula mpaka siku watayo fufuliwa viumbe. [79]
Maelezo ya chini[79] Iblisi akasema: Mola Mlezi! Nipe muhula, wala usinifishe mpaka Siku ya kufufuliwa viumbe.
Kiungo 38:79
80
قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ ٱلْمُنظَرِينَ
Mwenyezi Mungu akasema: Basi umekwisha kuwa miongoni mwa walio pewa muhula, [80]
Maelezo ya chini[80] Akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Basi wewe utaakhirishwa, utapewa muhula, mpaka siku ya wakati tunao ujua Sisi, nao ni kumalizika dunia.
Kiungo 38:80
81
إِلَىٰ يَوْمِ ٱلْوَقْتِ ٱلْمَعْلُومِ
Mpaka siku ya wakati maalumu. [81]
Maelezo ya chini[81] Akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Basi wewe utaakhirishwa, utapewa muhula, mpaka siku ya wakati tunao ujua Sisi, nao ni kumalizika dunia.
Kiungo 38:81
82
قَالَ فَبِعِزَّتِكَ لَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ
Akasema (Iblisi): Naapa kwa utukufu wako, bila ya shaka nitawapoteza wote, [82]
Maelezo ya chini[82] Iblisi akasema: Basi naapa kwa Ukubwa wako na Utukufu wako, kwa yakini nitawapoteza watu wote, isipo kuwa waja wako ulio wateuwa kwa ajili ya kukut'ii Wewe. Hao sina madaraka nao.
Kiungo 38:82
83
إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ ٱلْمُخْلَصِينَ
Isipo kuwa wale waja wako miongoni mwao walio khitariwa. [83]
Maelezo ya chini[83] Isipo kuwa waja wako ulio wateuwa kwa ajili ya kukut'ii Wewe. Hao sina madaraka nao.
Kiungo 38:83
84
قَالَ فَٱلْحَقُّ وَٱلْحَقَّ أَقُولُ
kasema: Haki! Na haki ninaisema. [84]
Maelezo ya chini[84] Akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Haki ndiyo yamini yangu na kiapo changu; na wala sisemi ila Haki. Bila ya shaka nitaijaza Jahannamu kwa jinsi yako ya kishetani na watakao kufuata katika vizazi vya Adam wote. Hapana khitilafu kwangu baina ya wafuasi na wanao fuatwa.
Kiungo 38:84
85
لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنكَ وَمِمَّن تَبِعَكَ مِنْهُمْ أَجْمَعِينَ
Bila ya shaka nitaijaza Jahannamu kwa wewe na kwa hao wote wenye kukufuata miongoni mwao. [85]
Maelezo ya chini[85] Akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: Haki ndiyo yamini yangu na kiapo changu; na wala sisemi ila Haki. Bila ya shaka nitaijaza Jahannamu kwa jinsi yako ya kishetani na watakao kufuata katika vizazi vya Adam wote. Hapana khitilafu kwangu baina ya wafuasi na wanao fuatwa.
Kiungo 38:85
86
قُلْ مَآ أَسْـَٔلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍۢ وَمَآ أَنَا۠ مِنَ ٱلْمُتَكَلِّفِينَ
Sema (Ewe Mtume) : Sikuombeni ujira juu ya haya, wala mimi si katika wadanganyifu. [86]
Maelezo ya chini[86] Ewe Muhammad! Waambie umma wako: Mimi sikuombeni ujira kwa ajili ya haya niliyo amrishwa nikufikishieni yaliyomo katika Qur'ani na Wahyi. Wala mimi si katika hao wanao jipamba na yasiyo kuwa yao, hata nijidai Unabii.
Kiungo 38:86
87
إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌۭ لِّلْعَـٰلَمِينَ
Hayakuwa haya ila ni mawaidha kwa walimwengu wote. [87]
Maelezo ya chini[87] Haikuwa Qur'ani ila ni ukumbusho na mawaidha kwa walimwengu wote.
Kiungo 38:87
88
وَلَتَعْلَمُنَّ نَبَأَهُۥ بَعْدَ حِينٍۭ
Na bila ya shaka mtajua khabari zake baada ya muda. [88]
Maelezo ya chini[88] Na hapana shaka nyinyi, mnao ikadhibisha Qur'ani, mtakuja jua karibuni hivi ukweli uliomo ndani yake wa ahadi, na maonyo, na khabari za mambo yatakayo kuja, na Ishara za ulimwengu.
Kiungo 38:88

Soma na usikilize kila siku kwenye programu ya Niyat, pamoja na nyakati za swala, kibla na mahali ulipofikia.

Pata Niyat bure